Mirathi Na Sheria Husika

Posted by: Roel Advocates Category: Article

  1. MIRATHI

Mirathi ni mali aliyoacha marehemu kwa ajili ya kurithishwa warithi wake halali. Sheria imeweka taratibu maalum zinazoongoza ukusanyaji, uangalizi, usimamizi, ugawaji na umiliki wa mali za marehemu pamoja, na kulipa madeni aliyoacha marehemu wakati wa uhai wake au gharama zitokanazo na mazishi yake.

Sheria zinazohusu urithi na wosia (mirathi) hapa Tanzania zimegawanyika katika sheria za mila, sheria za kidini na sheria za serikali. (Zitafafanuliwa hapo baadae)

  1. AINA ZA MIRATHI

Kuna aina kuu mbili za mirathi:

  1. Mirathi palipo na wosia: Mirathi ya aina hii inahusika ikiwa marehemu ameacha wosia, yaani tamko la maandishi au maneno yanayoweza kuthibitishwa na mashahidi, kwamba anataka mali, madeni yake yakusanywe, kutunzwa na hatimaye kurithishwa na/au kumilikishwa kwa nani na/au kwa namna gani. Kwenye huo wosia marehemu pia hutaja ni nani angependa awe msimamizi wa mali na/au madeni yake ikiwa ni pamoja na kuyakusanya na kuyatunza hadi hapo mali au kulipa madeni hayo yatakapomilikishwa. Endapo marehemu ameacha wosia na katika wosia huo amemtaja mtu atakayesimamia ukusanyaji wa mali na madeni na mgawanyo wa mali na/au malipo ya madeni ya marehemu, mtu huyo hupeleka maombi yake mahakamani na mahakama ikiridhia humthibitisha kuwa mtekelezaji wa wosia.

Mirathi pasipo na wosia: Pale ambapo marehemu hakuacha wosia kwa maandishi au tamko juu ya mgawanyo wa mali zake, warithi halali wa marehemu hulazimika kupendekeza kupitia kikao cha wana ukoo, mtu mmoja au zaidi kisha mtu au hao watu hupeleka maombi yao mahakamani na mahakama ikiridhia basi itawateua kuwa wasimamizi wa mirathi.

  1. HAKI YA KURITHI NA MAMLAKA YA KUSIKILIZA MASHAURI YA MIRATHI

Kwa ujumla mahakama ndio chombo pekee chenye mamlaka ya kutoa haki nchini Tanzania. Mamlaka haya yanatokana na Ibara ya 107A (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977. Kwa wepesi wa uelewa Ibara husika inasomeka kama ifuatavyo: –

107A. (1) Mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Mahakama.

Kwa msingi huo, mashauri yanayohusu mirathi, wosia na kusimamia mali zinazoachwa na marehemu ni jukumu la Mahakama kama inavyofanya katika aina nyingine za mashauri kama vile ya jinai na madai. Katika kutekeleza utoaji haki katika mashauri yanayohusu mirathi, usimamizi wake na hata mgawanyo wa mali za marehemu, Mahakama inaongozwa na sheria za nchi zilizotungwa na bunge kwa ajili ya madhumuni hayo. Hata hivyo mila, desturi, utamaduni, na dini ya marehemu huzingatiwa pia wakati wa mirathi kulingana na aina ya maisha ya marehemu enzi za uhai wake.

  1. HAKI YA KURITHI.

Haki ya kurithi ndio kiini cha hatua mbali mbali ambazo mwombaji au mrithi huzipitia ili kuhakikisha haki hiyo inapatikana. Haki ya kurithi inashabiiana na Ibara ya 24(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungao wa Tanzania ambayo inajenga dhana ya haki ya kumiliki mali. Mmiliki anapofariki, lazima apatikane mwingine wa kumikiki wa mali hiyo.

Upatikanaji wa haki ya kurithi unachagizwa na hatua za kuchagua msimamizi wa mirathi au mtekeleza wosia ambazo ni daraja tu la kufikia haki ya kurithi. Ugomvi na kutokuelewana kwa wanandugu au wanufaika wa mirathi huchochewa na kiu ya kulinda haki yao ya kurithi.

Endapo marehemu ameacha wosia, warithi watapata haki yao ya kurithi kwa mujibu wa wosia na pale ambapo hakuna wosia basi kuna sheria mahususi ambazo zinatoa haki ya kurithi kulingana na mila, desturi na dini.

Hivyo Mahakama hutumia sheria hizo zinazotoa haki ya kurithi kwa mujibu wa maisha ya marehemu kwa kuzingatia dini yake na mila.

  1. SHERIA ZINAZOTOA HAKI YA KURITHI TANZANIA

Haki ya kurithi nchini Tanzania inatamkwa na sheria kadhaa kama ifuatavyo hapa chini kutokana na asili ya mtu au imani yake ya dini.

Sheria hizo ni kama zifuatavyo: –

  • The Indian Succession Act 1865
  • Sheria ya Mila [The Customary Law (Declaration) (No.4) Order of 1963 GN No. 219 of 1967 read together with GN No. 436 of 1967]
  • Sheria ya Dini ya Kiislamu. [The Islamic Law (Restatement) Act, Cap 375 R. E 2002]
  • The Hindu Wills Act 1870
  • The Succession (Non-Christian Asiatic) Act.
  • The Law of the Child Act

Sheria Na. a) na Na. d) hapo juu zinatumika nchini kwa kupitia nyongeza ya II ya Sheria ya Judicature and Application of Laws Act, [Cap. 358 R.E 2002] (JALA) hivyo ni sehemu ya sheria za nchi.

  • The Indian Succession Act 1865: Sheria hii imerasimishwa kutoka sheria za India na chimbuko lake ni sheria za Uingereza ambazo zilitungwa mahususi kwa jamii ya waingereza nchini India ambao ni wakristo pekee dhidi ya waislamu na wahindu. Sheria hii inatumika kwenye mirathi yenye wosia na ile isiyo na wosia. Sehemu ya V ya sheria hii inaelezea juu ya haki ya kurithi ikijumuisha wajane, wagane na wanufaika wengine isipokuwa watoto wa nje ya ndoa.
  • The Hindu Wills Act 1870: Sheria hii inaongelea haki ya urithi kwa watu wenye asili ya Hindu ambao sio wakristo wala waislamu na pia jamii ambayo sheria ya Indian Succession Act haitumiki. Kimsingi sheria hii inaongelea juu ya kutengeneza wosia na taratibu za kupima uhalali wa wosia kwa watu ambao wanafuata sheria hii.
  • Sheria ya Mila yaani The Customary Law (Declaration) (No.4) Order of 1963 GN No. 219 of 1967, ikisomwa pamoja na GN No. 436 of 1967 imetokana na mamlaka ya kifungu cha 12(3) cha JALA. Katika tamko/sheria hii haki ya kurithi inaongelewa kwenye aya ya 30 ya nyongeza ya II ambapo haki ya kurithi hutegemea jinsia na umri. Kwa ujumla wake wanawake hawapewi haki sawa na wanaume ambapo kanuni ya 5 inawaweka wanawake daraja la chini pamoja na watoto.

Kimsingi sheria hizi zilitambua na kurasimisha kisheria mila na desturi za wananchi wa Tanzania ambao hawana asili ya Asia na Ulaya ambao katika maisha yao wameishi kwa kufuata na kuzingatia taratibu za mila, tamaduni na desturi zao. Sheria hii inatoa haki ya kurithi kwa wale ambao wameishi kwa kuzingatia mila na desturi katika jamii husika.

Kwa kufuata misingi hiyo, pale ambapo inathibitika na Mahakama kuridhika kuwa enzi za uhai wake marehemu aliishi kwa kufuata, kuzingatia na kuheshimu mila na desturi za kabila lake, basi mirathi itafuata sheria za mila za kabila/jamii hiyo kama zinavyotumiwa na wahusika.

Kwa sehemu kubwa sheria za urithi wa kimila zikitumika hufuata upande wa mwanaume ambapo warithi huwa ni watu wanaoangukia katika ngazi tatu kama ifuatavyo: –

  1. Ngazi ya kwanza; hii inalenga mtoto wa kiume wa kwanza kutoka katika boma/ nyumba ya kwanza kama marehemu alikuwa na ndoa ya wake wengi. Pia huangaliwa mtoto wa kiume aliyezaliwa kwanza kutoka boma/nyumba yoyote, endapo marehemu hakubahatika kuwa na mtoto wa kiume katika Boma/nyumba ya kwanza.
  2. Ngazi ya pili: Katika ngazi hii warithi au wanufaika ni watoto wote wa kiume waliosalia ambao hurithi sehemu kubwa kuliko watoto wa kike ambao huangukia katika ngazi ya tatu.
  3. Ngazi ya tatu: hii ni ya mwisho kabisa ambapo watoto wa kike hujumuishwa pamoja bila kujali tofauti zao za umri na au nafasi za mama zao katika ndoa. Mgao wao huwa sehemu ndogo kuliko mgao wanaopata watoto wa kiume. Hata hivyo endapo itatokea marehemu hakubahatika kupata watoto wa kiume, basi watoto wa kike huongezewa urithi.

ZINGATIO:  Sehemu kubwa ya mila na tamaduni za watanzania zimekuwa na mrengo wa kupendelea au kuegemea kwa wanaume zaidi na kubagua haki ya mwanamke katika kurithi au kumiliki mali. Ili kuweka usawa mbele ya sheria, mnamo mwaka 1999 Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ilifuta dhana nzima ya ubaguzi wa sheria za kimila. Kwa ufupi sheria hii ilileta usawa baina ya mwanaume na mwanamke katika kumiliki ardhi. Sheria imetamka kuwa; “… sheria yoyote ya kimila inayowanyima wanawake, watoto au watu wenye ulemavu uhalali wa kumiliki mali, kutumia au kupata ardhi, basi sheria hiyo ya mila itakuwa batili…”

Mila nyingi hazikuzingatia kabisa ushiriki au uchangiaji wa mjane katika kuchuma mali za familia ambazo mwisho wa siku hutambulika kama za mwanaume tu. Hata hivyo kwenye shauri la Maagwi Kimito vs Gibeno Werema [1985] TLR 132 (CA, Mahakama ya Rufani iliweka bayana kuwa sheria zote za kimila katika nchi hii lazima ziwe na hadhi sawa kwenye Mahakama kama sheria nyingine isipokuwa tu kama Katiba au sheria za nchi zitaelekeza tofauti. Kwa nukuu Mahakama ilisema: – “…The customary laws of this country now have the same status in our courts as any other law subject only to the Constitution and any statutory law that may provide to the contrary…”

Kuna mifano kadhaa ambapo Mahakama zetu za juu zimetoa miongozo juu ya sheria za mila katika mirathi. Kwenye kesi ya Violet Ishengoma Kahangwa & Jovin Mutabuzi vs Administrator General & Mrs Eudokia Kahangwa (1990) TLR 72 (CA), Mahakama ya Rufani pamoja na mambo mengine ilielekeza kuwa; “…that under paragraph 43 of the Local Customary Law (Declaration) (No.4) Order, 1963, G.N. No.436 as applied to the Bahaya tribe vide G.N. No. 605 of 1963, an illegitimate child cannot inherit from the father’s side upon his dying intestate…”

Kwa tafsiri rahisi Mahakama ya Rufani imesema kuwa katika mila za Wahaya mtoto wa nje hawezi kurithi mali za marehemu baba yake pale anapofariki bila ya kuacha wosia.

Mfano mwingine tunaupata kwenye shauri la Masudi Ally vs Chiku Masudi (1992) TLR 50 ambapo Mahakama Kuu ilisema: “…that under paragraph 26 of the 2nd schedule of the Customary Law Declaration 436/1963 only children of the deceased have the right to inherit from their deceased’s parents’ property… it is the children – them alone – of the Deceased that are customarily entitled to inherit the entire property, (without exception), of their late father. The appellant having been a complete stranger to the family of the Respondent’s late father, he is equally a stranger to the property of the Respondent’s late father…”

Kwa Kiswahili Mahakama Kuu imesema kuwa ni watoto wa marehemu pekee wanaoweza kurithi mali za marehemu baba yao. Mtu baki haruhusiwi kurithi chini ya sheria za mila.

Jambo muhimu la kuelewa na ama kuzingatia ni kuwa kwenye shauri la Violet Ishengoma Mahakama ya Rufani ilitafsiri haki ya kurithi kwa mtoto wa nje ya ndoa kwa kuzingatia sheria za mila pekee.

Hata hivyo kwa kwa upande mwingine na kwa kuzingatia kuzingatia Sheria ya Mtoto na shauri la Elizabeth Mohamed vs Adolf John Magesa, Probate and Administration Appeal No. 14 OF 2011 (unreported) HC Mwanza Mahakama Kuu imesema kuwa mtoto wa nje ya ndoa anayo haki ya kurithi mali za marehemu baba yake. Pia kwenye shauri la Judith Patrick Kyamba vs Tunsume Mwimbe & 3 Others, Probate and Administration Cause No. 50 of 2016 HC at Dar es salaam ambapo pamoja na mambo mengine Mahakama Kuu imekuwa na mtazamo kuwa mtoto hapotezi haki ya kurithi mali ya mzazi wake kwa kigezo cha kuzaliwa nje ya ndoa.

Kwa kuzingatia maamuzi ya Mahakama ya Kuu hadi sasa, (kwa kuwa bado maamuzi haya hayajatenguliwa na Mahakama ya Rufani) mtoto anastahili kurithi hata kama amezaliwa nje ya ndoa. Maamuzi haya ya Mahakama Kuu hayakinzani na maamuzi ya Mahakama ya Rufani kwenye shauri la Violet Ishengoma kwa kuwa sheria zilizotumika ni tofauti.

  • Sheria ya Dini ya Kiislamu: Sheria ya Kiislamu inatumika kwa wale wanaokiri au kuamini imani ya dini hiyo. Imani ya Kiislamu kuhusu mirathi ni kuwa mirathi ya peponi na duniani ni ya Mwenyezi Mungu. [Suraat Al-Imraan (2:180)]

Taratibu za kuendesha mirathi katika sheria hii zinajengwa kwenye dhana kuwa wanufaika wa mali za marehemu ni uhusiano wa karibu kwa kuzaliwa (consanguinity) au uhusiano wa ndoa.

Hata hivyo haki ya kurithi na taratibu zake zipo kwenye Kuruani Tukufu (The Holy Qur’an). Taratibu hizi zinapata nguvu ya sheria kutoka kwenye sheria ya The Islamic Law (Restatement) Act, ambapo kifungu cha 2 cha sheria kinampa Waziri wa Sheria kuandaa tamko la sheria ya Kiislamu kwenye jambo lolote kuhusu imani ya Kiislamu (The Statements of the Islamic law). Hata hivyo hadi sasa Waziri ametoa Tamko la Kiislamu kwenye sheria ya ndoa (Tamko la Sheria za Kiislamu la mwaka 1967, GN 222 of 1967) Hivyo hakuna tamko la aina hiyo kwenye sheria za mirathi.

Hii inamaanisha kuwa kwenye imani ya Kiislamu mirathi inafuata utaratribu ambao upo kwenye Kuruani Tukufu (The Holy Qur’an) pekee. Mistari inayoongelea mirathi katoka Qur’an tukufu ni pamoja na Surat Annisaa. [4:11, 12, 176]

 

Kwa mirathi yeyote ile, mgawanyo wa mali ya marehemu kwa mujibu wa Sheria ya Kiislamu, huzingatia mambo muhimu matatu yafuatayo, kwamba:

  • Mwenye mali awe alishakufa (maut al–muwarith)
  • Pawepo na warithi halali wa marehemu (hayat al-warith), yaani watoto wa marehemu ndugu wengine wa marehemu. Warithi hawa ni lazima wawepo na wawe ni warithi hakika wanaotambulika kisheria wakati wa mauti ya marehemu
  • Marehemu ameacha mali (al- tarikah I al–mauruth)
  • Urithi utokane na mali mali halisi na halali za marehemu na sio nje ya hizo.

Kabla ya mirathi lazima matatizo yafuatayo yawe yametatuliwa kwanza:

  • Madeni yanayokabili mali za marehemu
  • Gharama za Mazishi
  • Utatuzi wa madeni mengine
  • Wosia uwe umefuatiwa
  • Warithi halali

Kulingana na mafundisho ya dini ya Kiislamu, wanazuoni wote kwa ujumla wanaafiki kuwepo kwa makundi yafuatayo kuwa ndio warithi halali kwa mujibu wa dini ya Kiislamu:

  • As’hab Al – Furud: Hili ni kundi la watu wanaopata urithi wao kufuatana na muainisho wa bayana uliotolewa ndani ya Kuruani Tukufu. Hawa kwa kawaida wapo kumi na mbili (12).
  • Kati yao, wawili (2) hupatikana kwa njia ya mahusiano ya kinyumba yaani mke na mume, wengine hutokana na undugu wa damu na uhusiano wa ukaribu kidugu, yaani jamaa.

Kwa ujumla wao, ni kama ifuatavyo: (i) Mume, (ii) Mke, (iii) Mtoto wa kiume, (iv) Mtoto wa kike, (v) Mama, (vi) Dada, (vii) Kaka, (viii) Mpwa, (ix) Dada wa kambo, (x) Kaka wa kambo, (xi) Babu mzaa baba.

  • Asabah: Hawa ni wale wenye kupata urithi kutokana na albaki ya mali yote baada ya wale warithi waliobainishwa kwenye Qur’an kupata sehemu yao.
  • Hazina ya Umma: Kwa mujibu ya wanazuoni wa Kiislamu, kuna mgawanyiko wa mawazo katika kuthibitisha uhalali wa kuchukuliwa sehemu ya mali ya marehemu na kutolewa kama hazina ya umma. Mfano kundi linaloongozwa na Iman Hanafi na Hanbal, wanapinga mali za marehemu kupelekwa katika hazina kusaidia jamii. Lakini wale wenye mtazamo wa mawazo kama ya Malik na Shafii wanaafiki suala la mali ya marehemu kuchukuliwa na kurithishwa kwenye hazina ya jamii.

Mali za namna hii huwa ni mali ya jamii nzima na huwa chini ya msimamizi wake mkuu aliyechaguliwa na jamii yenyewe. Mfano katika serikali ya mapinduzi Zanzibar, mali zitolewazo kama Baitul Mal (haziina ya umma), zimewekwa chini ya uangalizi wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana.

  • Dhawl – Arham: hili ni lile kundi la wale ndugu wasiotokana na damu ya marehemu moja kwa moja.

Kwa kuondoa utata kifungu cha 4 cha sheria ya The Islamic Law (Restatement) Act kimeeleza kuwa tamko lolote litakalotolewa chini ya sheria hiyo litakuwa na nguvu kwenye mambo ambayo sheria za Kiislamu zinatumika kwa mujibu wa The Succession (Non- Christian Asiatics) Act, Cap. 28 R.E 2002, Kwa ujumla wake kifungu cha 6 kinatoa utaratibu wa kuendesha mirathi kwa mtu ambaye amekufa akifuata imani ya Kiislamu. Kifungu kinasema kuwa mirathi ya mtu huyo itafuata sheria za dini aliyokiri marehemu wakati wa uhai wake.

ZINGATIO:

  1. Izingatiwe kwamba mgawanyo wa mali kwa mujibu wa dini ya Kiislamu, hufuata matabaka kama yalivyobainishwa hapo juu.
  2. Kulingana na Sheria ya Kabidhi Wasii Mkuu, endapo mtu atakufa bila kuwa na mrithi, au kwamba mali yake inaweza kupotea, basi hiyo mali itawekwa chini ya Kabithi Wasii Mkuu, na endapo utapita muda wa miaka kumi na mbili (12) bila mtu yeyote kudai kitu chochote kuhusu mirathi hiyo, basi Kabidhi Wasii Mkuu ataihamishia mali hiyo Serikalini.
  • Sheria ya The Succession (Non-Christian Asiatics) Act, [ 28 R.E 2002]. Sheria hii inatumika na kutoa haki ya kurithi kwa watu ambao si Wakristo (Non – Christian Asiatic). Utaratibu wa haki ya kurithi unazingatia sheria ya dini ambayo marehemu alikuwa amekiri. Sheria hii inalinda haki ya mirathi hasa pale ambapo marehemu anakuwa ametengwa (excommunicated) kwenye imani yake.
  • Sheria ya Mtoto No. 21 of 2009, Kifungu cha 10 cha sheria hii ni kosa kisheria kumnyima mtoto haki yake ya kurithi mali za wazazi wake. Pamoja na kuwa mtoto hajafikia umri wa mtu mzima (miaka 18) sheria hii inatoa msimamo thabiti kuwa mtoto asinyimwe haki ya kurithi. Mahakama Kuu ilitilia mkazo kwenye haki ya kurithi kwa mtoto kwenye shauri la Elizabeth Mohamed ambapo ilisema hata mtoto wa nje ya ndoa anayo haki ya kurithi.

 

  1. TARATIBU ZA KUFIKIA HAKI YA KURITHI

Katika kufikia haki ya kurithi ni lazima kufuata sheria zilizopo kwa ajili hiyo. Kuna sheria ambazo zinatumika Mahakama ya Mwanzo na nyingine zinatumika Mahakama za juu. Sheria hizi ni pamoja na: –

  • Kanuni za Usimamizi wa Mirathi Mahakama ya Mwanzo (The Primary Courts (Administration of Estates) Rules GN. 49 of 1971);
  • Sheria ya Usimamizi wa Mirathi (The Probate and Administration of Estates Act Cap. 352 R.E. 2002);
  • Kanuni za Mirathi (The Probate Rules, GN. 369 of 1963);
  • Sheria ya Mahakama za Mahakimu (The Magistrates’ Courts Act, Cap. 11 R.E. 2002);
  • Sheria ya Usimamiaji Haki na Matumizi ya Sheria (Judicature and Application of Laws Act, Cap. 358 R.E 2002);
  • Sheria ya Ukomo wa Muda (The Law of Limitation Act, Cap. 89 RE 2002);
  • Sheria ya Mtoto (The Law of the Child Act, No. 21 of 2009)

 

  1. Uchaguzi wa Sheria ya Kutumia

Matatizo na malalamiko mengi yasingetokea juu ya sheria za mirathi na ugawaji wa mali za marehemu kama jamii ingejua ni sheria ipi itumike juu ya mali zao wakati hawapo duniani. Uandaaji wa wosia na uchaguzi wa sheria ya kutumika wakati wa usimamizi na hatimaye ugawaji wa mali za marehemu ni jambo nyeti sana.

7.1 Uchaguzi Kulingana na Maisha ya Marehemu

Kama tulivyoona hapo awali, sheria imetambua na kuruhusu kutumika kwa mila na desturi za jamii husika katika kutatua migogoro mbalimbali ya jamiihiyo. Kwa upande wa mashauri yanayohusu mirathi mfano mzuri tunaupata katika kesi ya Innocent Mbilinyi (Deceased), (1969) HCD No. 283. ambapo katika kesi hii mwanaume mmoja wa Kingoni alimuoa dada wa Kichaga kwa kufuata ndoa ya kikristo na wawili hao walikuwa wanaishi mkoani Dar es salaam. Marehemu (Innocent) aliondoka nyumbani kwao Songea tangu akiwa na miaka 7 na amepata masomo yake hadi elimu ya juu akiwa nje ya mkoa wake. Mara chache amekuwa akitembelea nyumbani Songea au Moshi. Wawili hao walibarikiwa watoto watatu katika maisha yao ya ndoa. Wakati wa kusikiliza shauri la mirathi mjane alisisitiza sheria ya serikali (statutory law) itumike ili aweze kupata haki yake ya kurithi. Kwa upande mwingine kaka wa marehemu alitaka sheria ya mila itumike ili mjane asipate urithi kabisa.

Mahakama Kuu (Georges, C.J) aliamua kuwa, marehemu aliachana na maisha ya kimila kwa kuishi kama mkristo na kutofuata taratibu za mila na desturi. Mahakama iliendelea kusema kuwa kuna ushahidi wa kujitosheleza kuwa marehemu alijitenga na familia yake na hata watoto wake hawana muunganiko na mambo ya mila, hivyo sheria ya serikali ilitumika.

Mfano mwingine tunaupata katika kesi ya George Kamwenda vs. Fides Nyirenda, [1981] TLR 211 katika shauri hili marehemu Merten Kumwenda alikuwa raia wa Malawi aliyeishi wilaya ya Temeke, Dar es salaam. Baada ya kifo chake marehemu aliacha nyumba moja. Mjane alitaka kurithi nyumba kwa kupitia sheria ya serikali. Hata hivyo kaka wa marehemu alipinga hilo akitaka sheria ya mila itumike ili mjane asipate urithi wa nyumba hiyo bali iuzwe fedha zitakazopatikana zigawanywe kwa kaka, dada, wazazi na watoto wa marehemu. Mahakama ya Mwanzo iliamua kutumia sheria za mila lakini Mahakama ya Wilaya iliamua kutumia sheria ya serikali. Shauri lilipofika Mahakama Kuu, (Kisanga, J.) iliamuliwa kuwa shauri lianze upya kwa kusikilizwa kwa kuwa Mahakama za chini zilipotoka/ zilikosea kisheria na kimantiki kwa kutokuchukua jitihada za kutosha kuchunguza maisha ya marehemu wakati wa uhai wake ili kubaini ni sheria gani itumike katika shauri hilo.

Kwa kuzingatia mifano miwili ya kesi hapo juu haina shaka kusema kuwa ili kutambua sheria gani ya kutumia kuendesha shauri la mirathi (endapo marehemu hakutamka) basi Mahakama lazima ijiridhishe kikamilifu aina ya maisha ya marehemu enzi za uhai wake. Hata hivyo, pamoja na kuwepo kwa dhana ya jumla kuwa mwafrika anayeishi kijijini au mjini sheria ya kutumia ni ile ya mila kama ilivyoamuliwa kwenye kesi ya Abdallah Shamte vs. Mussa, (1972) H.C.D. No. 9 dhana hii inaweza isitumike endapo itabainika kuwa marehemu hakuishi kwa kufuata mila na desturi za jamii yake.

7.2 Uchaguzi Kulingana na Matakwa ya Marehemu

Pale inapotokea marehemu alikuwa akifuata Imani ya dini ya Kiislamu mara nyingi hutokea mgongoro juu ya sheria ipi hasa itumike kuendesha shauri la mirathi kati ya sheria ya mila, sheria ya kiislamu au ile ya serikali. Kifungu cha 88 cha Sheria ya Mirathi kinaongelea utaratibu wa kufuata.

Imeandikwa na;

Eliaman Daniel, Wakili

ROEL ER & CO. ADVOCATES

6th Floor, NSSF – Mafao House Ilala

Along Uhuru Street,

P.O. Box 13496,

Dar es Salaam, Tanzania

Email: eliaman@roeleradvocates.co.tz

Mobile: +255 766 016 307/+255 684 128 184

Share this post


Are You Looking for

Experienced Attorneys?

Get a Free Consultation Right Now

× How can I help you?